Jumanne, 29 Novemba 2016

Utafiti wa Kielimu, Upimaji na Tathmini | Sehemu ya I






1. Tathmini ni nini?
Ni utaratibu wa kupima na chukunguza hali halisi kwa lengo la kupata data zitakazo mwezesha mwalimu au mtahini kufanya maamuzi yanayohusu urekebishaji au uboreshaji wa mambo mbalimbali katika elimu.
2. Kutahini ni nini?
Ni tendo la kutoa seti ya maswali yenye kiwango na mpangilio unaokubalika ili yajibiwe na mtahiniwa ili kupima kiwango fulani cha elimu alichojifunza.
3. Upimaji wa Kielimu ni nini?
Ni tendo la kutafuta ni kwa kiasi gani mwanafunzi amepata maarifa na stadi alizofundishwa kufuatana na malengo ya ufundishaji.
4. Mfiko ni nini?
Mfiko ni maksi inayoonesha tofauti kati ya maksi ya juu kabisa na maksi ya chini kabisa katika seti ya maksi za watahiniwa.
5. Ni Zana zipi za msingi zitumikazo katika upimaji wa haraka za kufundisha na kujifunza?
Zana zitumikazo katika upimaji wa haraka za kufundisha na kujifunza ni kama vile;
·         Maswali
·         Mazoezi
·         Majaribio na
·         Mitihani
·         Eleza kwa kifupi matumizi ya matokeo na majaribio
6. Mitihani ni upimaji unaotolewa baada ya mwanafunzi kumaliza ngazi Fulani ya elimu. Mtihani hutolewa katika muda maalum na muda huo hauna budi kujulikana kwa mtahiniwa.
7. Fafanua Matumizi ya Matokeo ya Mitihani
·         Hupima na kutathmini maendeleo ya mwanafunzi katika ngazi Fulani ya elimu.
·         Inatathmini ubora wa elimu inayotolewa
·         Inatathmini ubora wa mbinu na njia zinazotumika katika ufundishaji
·         Hutumika katika kufanya maamuzi ya kielimu (maamuzi ya kielimu ni kama uchaguzi kuingia ngazi nyingine ya elimu au kujifunza kozi fulani)
·         Hupima na kutathmini ufanisi wa Walimu na Mitaala
·         Husaidia kuleta ushindani katika kujifunza
8. Majaribio ni nini?
Majaribio ni maswali yanayopima kama mada kuu iliyofundishwa imeeleweka. Majaribio yanayotolewa huwa ya masomo mengi na hutolewa katika muda maalum kama vile mwisho wa kufundisha mada moja, mwisho wa juma, mwisho wa mwezi au mwisho wa muhula. Lakini hutegemea zaidi na mwalimu amejipanga vipi kufanya tahmini ya ufundishaji wa somo lake.
9. Eleza kwa ufasaha Matumizi ya matokeo ya Majaribio
·         Humwezesha mwalimu kuona kwamba malengo ya mada zilizofundishwa yamefikiwa.
·         Humsaidia mwalimu kujua kiwango cha uwezo wa wanafunzi katika mada iliyofundishwa.
·         Humsaidia mwanafunzi kuweza kutafuta mbinu bora zaidi za kujifunza na kutumia vizuri wakati (muda) wake na kupunguza kucheza.
·         Humsaidia mwanafunzi kujilinganisha na wanafunzi wenzake.
·         Husaidia kusanifu alama za mtihani wa mwisho.
·         Hutumika kurekodi maendeleo ya mwanafunzi.
10. Tunapotoa zoezi au jaribio au mtihani, je tunapima mafanikio ya mwanafunzi au tunapima utendaji wa wanafunzi? Eleza:
Katika ufundishaji na kujifunza kwetu tunapima vyote viwili, mafanikio ya wanafunzi na utendaji wa wanafunzi. Hatuwezi kutenganisha upimaji wa mafanikio na upimaji wa utendaji.
Baada ya kufundisha somo au mada Fulani upimaji kiasi gani wanafunzi wameelewa hufanyika. Kwa maneno mengine, tunapima wanafunzi wanaweza kufanya nini kutokana na wanavyofundishwa. Kumbuka kuwa tunapima ngazi ya chini na ngazi ya juu za upeo wa akili (kumbukumbu, ufahamu, uchambuzi, uunganisho na tathmini). Wakati wa kutoa ripoti za maendeleo ya wanafunzi kwa kawaida ni vizuri kutumia utendaji wa wanafunzi.
Hatumtumii mzazi matokeo ya mwanafunzi bali maendeleo ya utendaji.
11. Taja manufaa ya utayarishaji wa jedwali la mtawanyo katika kutahini (table of specification):
Manufaa ni haya yafuatayo;
·         Stadi zote zitakiwazo na jamii husisitizwa,
·         Maswali ya aina mbalimbali humsaidia mwanafunzi/mtoto kukua kimwili, kiakili na kimwelekeo.
·         Maswali hayo hupima kwa ukamilifu zaidi maendeleo ya tendo la kufundisha au kujifunza.
·         Utungaji wa maswali hayo mbalimbali humwongezea mwalimu upeo wa taaluma na uthabiti wa kina chake.
·         Njia hiyo ya utungaji wa maswali inakidhi na huwakilisha mada nyingi zaidi zilizomo katika muhtasari wa shule za msingi kwa wakati mmoja.
12. Ni mambo gani muhimu yanayopaswa kuzingatiwa katika muundo wa mtihani?
·         Malengo ya kujifunza
·         Njia au mbinu za kujifunzia
·         Malengo ya kutahini
13. Taja aina nne (4) za kutathmini katika Elimu.
·         Tathmini ya kupima uwezo wa kumudu kuanza masomo mapya
·         Tathmini ya kuendelea
·         Tathmini ya kudodosa
·         Tathmini ya mwisho/tamati
14. Maksi anayopewa mwanafunzi baada ya kufanya jaribio au mtihani huitwaje?
Alama anayopata mwanafunzi hata kabla haijarekebishwa huitwa alama ghafi
15. Taja madhumuni manne (4) tu ya upimaji wa maendeleo ya mwanafunzi:
·         Kujua/kufahamu maendeleo ya mwanafunzi kitaaluma
·         Kubaini matatizo ya wanafunzi katika kujifunza
·         Kusaidia kupata wanafunzi wa kuendelea na masomo ya juu zaidi
·         Ni kigezo kinachotumika katika utoaji wav yeti mwishoni mwa kozi ya mafunzo maalumu au baada ya kumaliza kiwango fulani cha elimu.
·         Taja ni hatua zipi mtafiti anapaswa kuzifuata katika kufanya utafiti?
16. Hatua atakazozizingatia mtafiti katika kufanya utafiti ni hizi zifuatazo;
·         Kutambua tatizo au suala la utafiti
·         Kuandika muswada wa utafiti
·         Kuandaa zana za kukusanyia data
·         Uchanganuzi na tafsiri ya data
·         Uandikaji wa ripoti ya utafiti
17. Ni mambo gani Mtafiti anayazingatia pindi anapohitaji kufanya uchanganuzi wa data?
Katika uchanganuzi wa data Mtafiti azingatie mambo yafuatayo;
·         Kuwepo uhusiano kati ya data na malengo
·         Kila data lazima ipate tafsiri yake
·         Kila data iwe na jibu la swali au dhanio kama lilivyokua kwenye malengo
·         Data zichanganuliwe na kutafsiriwa kikamilifu
·         Data zinaweza kupangwa kwa kutumia chati, majedwali, grafu na takwimu zikiambatana na maelezo, Mtafiti aeleze sababu iliyomfanya atumie aina hiyo mahsusi ya takwimu.
18. Ni hatua zipi mwalimu azifuate katika utungaji wa jaribio au mtihani?
Hatua zifuatazo mwalimu analazimika kuzifuata wakati wa kutunga maswali ya mtihani;
·         Mwalimu anatakiwa kutayarisha jedwali la kutahini (table of specification)
·         Mwalimu atunge maswali ya mtihani ikiwa utayarishaji wa jedwali la kutahini utakua umekamilika
·         Upangaji wa maswali katika mtihani
·         Utayarishaji wa mwongozo wa usahihishaji
19. Fafanua kwa ufasaha aina za upimaji katika Elimu ya Awali.
·         Upimaji wa awali
Upimaji huu unafanyika kabla mtoto hajaanza shule au pale tu anapoanza shule. Unasaidia kubainisha kama mwanafunzi ana tatizo lolote linaloweza kumzuia au kumkwamisha katika kujifunza kwake.  Pia upimaji huu utamsaidia mwalimu na mzazi kufuatilia matatizo ya mtoto, vipaji alivyonavyo na Historia ya mtoto na familia yake.Taarifa za upimaji huu zinaweza kutokana na hojaji za mzazi, kumchunguza mtoto na jinsi mtoto anavyojieleza.
·         Upimaji endelevu
Upimaji huu hufanyika kwa kutumia zana mbalimbali za upimaji, ni upimaji unaofanyika wakati mafunzo yanaendelea; mfano mazoezi, kadi za maendeleo ya mtoto, vitabu vya kumbukumbu mbalimbali za watoto, taarifa ya afya ya kila mwezi, mkoba wa kazi za uchunguzi wa vitendo vya masomo na fomu ya kumbukumbu ya kazi za kila siku za mtoto.
·         Upimaji tatuzi/gunduzi
Upimaji huu nalenga katika kutafuta kwa undani sababu zinazofanya mtoto asishiriki katika vitendo vya ujifunzaji na michezo. Upimaji huu hufanywa wakati mwalimu anaelekeza watoto na kuona kuwa wapo watoto ambao hawashiriki katika ujifunzaji au hawaelewi kinachoendela wakati wa ufundishaji na ujifunzaji.
·         Upimaji tamati
Aina hii ya upimaji kwa watoto hufanyika kwa kuunganisha taarifa zote tangu upimaji awali, endelevu na tatuzi ili kupata taarifa sahihi ya mabadiliko ya mtoto katika nyanja zote za kiakili, kimwenendo, afya, na ujifunzaji.Upimaji huu hufanyika mwishoni mwa mafunzo au muhula. Lengo la upimaji tamati ni kuangalia kiwango cha mafanikio kwa ajili ya kuendelea na mafunzo ngazi inayofuata.
Kwa kuzingatia upimaji wa maendeleo ya mtoto katika elimu ya awali hakuna ulinganifu wa matokeo unaofanyika wala mitihani inayotolewa kwa ajili ya kumpima mtoto. Bali upimaji hufanyika kwa kila mtoto kulingna na maendeleo yake kwa kufuatilia mabadiliko ya mtoto kiakili, kiafya, mwenendo na ujifunzaji tangu anapoanza mafunzo hadi mwisho wa mafunzo.
20. Ni nini Madhumuni na Umuhimu wa Upimaji katika Elimu ya Awali?
Madhumuni ya kupima uelewa wa mwanafunzi katika Elimu ya Awali ni:
·         kuamsha ari ya watoto kujifunza zaidi
·         kujua maendeleo watoto kiakili, kimwenendo, kitabia na kistadi
·         kumpa mwalimu mwelekeo wa kuboresha ufundishaji
·         kutoa taarifa ya maendeleo kwa wazazi au walezi
·         kutoa taarifa za maendeleo ya elimu kwa taifa.
                                               Sir ALMASI