Jumamosi, 14 Januari 2017

Mwongozo wa mwalimu anayefundisha darasa la awali






Mwongozo wa mwalimu anayefundisha darasa la awali …ALMASI MICHAEL
SIKU zote kunazungumzwa masuala ya elimu ya awali na umuhimu wake, lakini kwa bahati mbaya elimu hii haitiliwi maanani na ndiyo maana ukiwauliza watu 10 majina ya walimu wao wa awali ni wawili tu watakaokumbuka.
Katika makala ya leo nitazungumzia umuhimu wa elimu ya awali kwa kuangalia wanafalsafa makini walisema nini kuhusu elimu hii, lakini kwanza tujikumbushe mwalimu wa elimu ya awali ni nani?
Mwalimu wa elimu ya awali anatakiwa awe na msingi mzuri wa kitaaluma na kitaalamu ili  aweze kutoa elimu iliyo bora na kukidhi mahitaji ya watoto katika kujifunza.
Aidha, ufundishaji na kujifunza kwa watoto hutokea katika njia mbalimbali— rasmi na zisizo rasmi— hivyo mwalimu wa shule ya awali anahitaji maarifa na stadi za nyongeza ili kuwa mbunifu ili kila mtoto apate msaada unaostahili.
Mtazamo wa elimu ya awali
Elimu ya awali ni elimu ambayo inatolewa kwa ajili ya watoto wenye umri unaoanzia miaka 5-6. Lengo ni kuwajengea watoto msingi mzuri wa kielimu ili kujiunga na elimu ya msingi.
Katika shule hizi watoto hujifunza kwa kiasi kusoma, kuandika na kuhesabu. Wakiwa shuleni watoto hujifunza ushirikiano na watu wengine, tabia njema, kazi za mikono na mambo mengine yanayowasaidia katika makuzi.
Umuhimu wa elimu ya awali
Utafiti unaonyesha kuwa utoaji wa elimu bora na stadi mbalimbali katika umri wa miaka 0-6 huchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya mtoto katika maisha yake yote.
Vilevile, elimu hii husaidia kubaini matatizo mbalimbali ya watoto mapema ili wapatiwe msaada mapema kabla tatizo halijawa kubwa. Pia taarifa hizi husaidia serikali kubuni mipango ya kuwasaidia watoto hawa mapema.
Historia na maendeleo ya elimu ya awali Tanzania
Elimu ya awali nchini bado haijapiga hatua kubwa, hata hivyo katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na kukua kwa kasi kwa uanzishwaji wa shule za awali.
Elimu hii pia haijakua sana katika sehemu za vijijini ambako ni sehemu chache mno zenye shule za awali kutokana na upungufu wa walimu na mwamko duni wa wazazi.
Uamuzi wa hivi karibuni wa serikali wa kuwa na shule ya awali katika kila shule ya msingi ya serikali huenda ukachochea zaidi ukuaji wa elimu hii katika siku za hivi karibuni.
Elimu ya awali ilianza mwaka 1940 wakati wa kipindi cha ukoloni. Wakati huo elimu ya awali ilitolewa zaidi na taasisi za kidini hasa zile za Kikristo na Serikali ya Kikoloni kwa watoto wa tabaka maalumu.
Baada ya uhuru mwaka 1961, serikali ilitoa nafasi kwa taasisi mbalimbali ili kuanzisha na kutoa elimu ya awali kwa kufuata miongozo iliyowekwa.
Mwaka 1982 ripoti ya Tume ya Rais Julius Nyerere, ilipendekeza kuwa elimu ya awali iingizwe katika mfumo rasmi wa elimu, wizara ya elimu na utamaduni ilishauriwa iandae miongozo na vifaa vya kufundishia na kujifunzia pamoja na kutoa mafunzo kwa walimu wa elimu ya awali.
Miongozo ilitayarishwa mwaka 1991 na wizara ya elimu lakini kwa kuwa hakukuwa na chombo cha kufuatilia utekelezaji wake, shule nyingi zilitoa elimu ya awali bila kuzingatia viwango vinavyostahili.
Mwaka 1995, Sera ya Elimu na Mafunzo ilitolewa na kuelekeza kuwa elimu hii itatolewa kwa watoto wa miaka 5-6 na itasimamiwa na wizara.

Nadharia mbalimbali kutoka kwa wanafalsafa kuhusu elimu ya awali
MARIA MONTESSORI (1870- 1952)
Alizaliwa Italia; alikuwa mwanamke wa kwanza nchini humo kuwa daktari wa magonjwa ya watoto na magonjwa ya akili.
Katika ugunduzi wake, alingundua kuwa watoto waliovia akili wanaweza kufunzwa kwa kutumia vifaa vya kuchezea wanavyovipenda. Aliamini kuwa tatizo la kuvia akili ni la kielimu na sio la tiba.
Montessori, aliamini kuwa elimu ya mtoto ni lazima ianze mapema sana kwa sababu umri wa mtoto  kati ya kuzaliwa  hadi miaka sita ni muhimu sana kwa ujenzi wa haiba yake.
Alipendekeza mwalimu atumie vifaa vingi katika ufundishaji, vifaa hivyo viwe ni vile vinavyokuza tabia ya udadisi na ugunduzi, vinavyompa nafasi ya utendaji na vinavyomwezesha mtoto kufanya majaribio, kutatua vikwazo, ujasiri, kuuliza na kujibu maswali, kupenda kufaulu, kujiendeleza na kumpa msukumo wa kujitegemea katika utendaji.
Mwanafalsafa huyo hakuishia hapo, bali alibuni michezo ya kujifunzia, alitumia vifaa vya kuchunguza ambavyo humpatia mtoto maarifa na hapo hapo kukuza stadi wakati anapovichezea.
Kuhusu vyumba vya madarasa ya awali, alipendekeza vigawanywe katika vyumba vingi na kila chumba kiwe kwa ajili ya kufanyia shughuli maalumu tofauti, watoto wawe huru kutembea na kuingia kila chumba wakitakacho bila kizuizi.
Wanafunzi wajifunze kwa kushirikiana na hali inayotakiwa mle vyumbani iwe ya kuheshimu haki na kazi za kila mtu.Watoto wadogo wajifunze kutoka kwa wenzao walio wakubwa, vifaa vilivyomo katika nyumba kwa mfano viti vya kukalia viwe vidogo kama walivyo watoto wenyewe.
MONTESSORI, anajulikana sana kwa kuwa mtu aliyeanzisha njia ya kuwafundisha watoto wadogo.Njia yake ya kufundishia watoto wadogo aliigawa katika sehemu kuu zifuatazo:
  1. Elimu inayohusu ukuzaji wa stadi mbalimbali za misuli ya watoto. Elimu hii ni nzuri kwa kumsaidia mtoto aweze kukuza stadi zake na kufikia upeo wa juu katika kutumia viungo vya mwili. Ili kufikia hali hii, wanafunzi wafanye mazoezi mbalimbali ya kutembea na kupumua.
Pia, alitumia elimu ya mazoezi yanayohusiana na maisha ya kila siku ya mtoto kwa mfano usafi wa mwili, usafi wa mazingira ya ndani na nje.
  1. Elimu inayohusu ukuzaji wa milango ya fahamu, mazoezi aliyoyapendekeza kwa watoto ni yale ya kuwasaidia watoto kuweza kutofautisha  kati ya uwingi na ubora wa kitu, mazoezi yanayotumiwa  katika elimu hii ni yale ya kuona na kusikia.

  1. Elimu inayohusu weledi, mazoezi ya kuwapa wanafunzi ni yale ya kumtayarisha mtoto kusoma kuandika na kuhesabu, kwa mfano mtoto huanza kugusa, kuangalia, kuandika na hatimaye kusoma.

Vifaa ni vya lazima sana kwa kukuza elimu ya aina hii, vifaa hivyo ni kama vile shanga za rangi mbalimbali, vizibo vya chupa, vipande vya miti vilivyoandikwa namba, alfabeti zinazoweza kusogezwa au mbegu za mimea.

JEAN JACQUES ROSSEAU (1712-1778)
Alizaliwa mwaka 1712 katika mji wa Geneva huko Uswisi ambako alipata mafunzo yake ya awali kutoka kwa baba yake na baadaye kutoka kwa mkufunzi aliyeajiriwa kumfundisha.
ROSSEAU alikuwa na mwelekeo wa kuamini kuwa kwa asili watoto huzaliwa na tabia nzuri na kwamba ni mazingira ndiyo yanayowafanya kuwa na tabia mbaya.
Alisisitiza njia bora ya kuwaelimisha  watoto ni kuwaweka katika hali ya asili ambayo itamwezesha kukuza tabia, silika zao za uwezo bila kuathiriwa na mazingira.
Aligawanya maisha ya mtoto katika hatua nne;
  1. Hatua ya kwanza ni ya mtoto mchanga. Huu ni wakati mtoto anapojenga mazoea na tabia njema, ni wakati unaofaa kumwongoza mtoto kutawala maono yake.
  2. Hatua ya pili ni wakati wa kujifunza namna ya kutumia milango yake ya fahamu au maarifa.
  3. Hatua ya tatu ni mwanzo wa uvulana au usichana, hiki ni kipindi cha akili mtoto anapotumia akili yake juu ya vitendo anavyofanya.
  4. Kipindi cha nne ni uvulana au usichana mpevu (baada ya miaka 15), hiki ni kipindi cha fikra za kiroho, hapo mtoto anatambua hasa mema na mabaya.
ROSSEAU alieleza umuhimu wa mtoto kuwa kitovu cha elimu ili kumpa hali nzuri ya maisha. Alisisitiza kuwa elimu lazima imsaidie mtoto kuwa huru na mwenye furaha, elimu imsaidie mtoto kukuza haiba nzuri, na ili elimu ifikie malengo haya lazima itolewe kufuatana na hali na hatua za kukua kwa mtoto.
Mtoto afundishwe namna ya kujifunza na kutatua matatizo katika mazingira malimbali, alisisitiza kuwa elimu ni haki ya watoto wote ni chombo kinachoweza kuyatawala mazingira ya mtoto.
Alishauri kuwa ufundishaji  uende sambamba na hatua za ukuaji wa mtoto, uzingatie upevu na utayari wa mtoto katika kujifunza.
Njia bora za kufundishia ni zile zinazomsaidia mtoto kutumia milango mingi ya fahamu inavyowezekana. Ili kufanikiwa katika jambo hili mwalimu atumie zana za kufundishia hasa kwa kutumia vitu halisi.
Kwa mujibu wa mwanafalsafa huyu, elimu lazima izingatie mahitaji ya maadili, katika falsafa ya elimu ya kujitegemea ufundishaji wa maadili umezingatiwa kwa kuwafundisha wanafunzi masomo ya siasa na dini.
JOHN DEWEY
Huyu alizaliwa mwaka 1859  huko Vermont, Marekani na alifariki mwaka 1952 akiwa na umri wa miaka 93. Mwanafalsafa Dewey, aliandika mengi na kufanya mengi yaliyomtambulisha kidunia kuwa ni mtaalamu wa falsafa na mwalimu hodari hasa katika nadharia inayohusu malezi ya watoto.
Kutokana na kazi ya Dewey zilianzishwa shule zilizojulikana kama  shule za maendeleo, na malezi
yaliyotolewa yakaitwa malezi ya maendeleo.
Akiwa jimbo la Michigan, Dewey alianzisha kituo cha watoto wadogo alichokiita shule ya maabara mwaka 1896, alikusudia shule hiyo itoe nafasi ya kufanya utafiti na majaribio juu ya namna ya kujifunza.
Dewey alisisitiza kuwa elimu haiwezi kutengwa na jamii, kwa hali hiyo basi, elimu ni njia ambayo jamii huitumia katika kulinda, kuendeleza na kuhifadhi utamaduni wake.
Madhumuni ya elimu basi ni kutayarisha na kutoa raia walio bora na wanaoweza kuitumikia jamii yao kikamilifu.
Dewey aliamini kuwa katika kutenda au kufanya shughuli fulani, wanafunzi wanaweza kuelewa mambo vizuri zaidi. Alisisitiza kuwa maarifa hupatikana kutokana na shughuli wazifanyazo watoto.
Kuhusu suala la kujifunza, Dewey alitaja mambo ambayo ni muhimu kuzingatia wakati wa kumfundisha mtoto. Mambo hayo ni haya yafuatayo;
  1. Mwanafunzi lazima awe katika mazingira halisi ya aina ya uzoefu anaotakiwa kupata.
  2. Lazima kuweko na tatizo la kweli linaloamsha na kuchochea mawazo na ari ya mwanafunzi ya kutatua matatizo.
  3. Mwanafunzi lazima afanye uchunguzi na atafute au akusanye data za kumsaidia katika kulitatua tatizo lake.
  4. Ni lazima ajaribu kutafuta ufumbuzi mbalimbali wa tatizo hilo.
  5. Ni lazima apate muda wa kufanya majaribio kuona kama mawazo au dhanio alizozipata ni kweli zinaweza kuwa na uthibitisho wowote.
Dewey alilisisitiza kuwa shule iwe kaya njema ambamo mtoto atafundishwa maadili yote ya jumuiya yake, na kumjenga kimwili na kiroho.
 FRIEDRICH  FROEBEL
Froebel anashika nafasi ya pekee kati ya wataalamu wa mambo ya malezi, ijapokuwa mawazo yake makuu yalifanana na yale ambayo ROSSEAU alikuwa amekwisha kuyaandika.
Alizaliwa Ujerumani mwaka 1782 katika kijiji kilichokuwa katika msitu wa Turingia. Akiwa kijana bado alifanya kazi chini ya uangalizi wa Bwana Misitu na kwa nafasi hiyo alijipatia moyo wa kupenda uoto wa asili juu ya sura ya nchi, na pia kupenda maumbile ya asili ya nchi.

Sifa kuu ya Froebel imo hasa katika kuzua wazo la kuwa na shule za Chekechea (Kindergarten). Jina hili la Kindergarten ambalo lina maana ya “bustani ya watoto”  ndilo hasa lililoeleza imani na msimamo wa Froebel juu ya malezi.
Yeye alimlinganisha mtoto na mmea mchanga, na kazi ya mwalimu akailinganisha na kazi ya mkulima bustani ambaye wajibu wake ni kutengeneza mazingira yanayofaa ili mmea ukue wenyewe hata kufikia kikomo chake.
Mawazo yake kuhusiana na elimu na jinsi ya kumuandaa mtoto kielimu ni haya yafuatayo:
Froebel alipendekeza pawe na umoja katika mambo yanayofundishwa na kutaka tuepuke hatari ya kuyagawa masomo katika sehemu ndogondogo zisizohusiana, kwa mfano yeye alihimiza kuwa mitaala ya masomo ionyeshe umoja.
Aliwalaumu pia walimu wa vyuo vikuu ambao walikuwa wameligawa somo la malezi katika sehemu nyingi ili waandike vitabu.
Alisema pia katika shughuli ya malezi, uhuru wa mtoto ni muhimu uzingatiwe, “Sisi binadamu tunapotunza mimea na wanyama tunawaachia nafasi ya kujimudu na pia muda wa kukua.
“Lakini mtoto wa binadamu tunamfanya kama kipande cha nta au donge la udongo, ambalo tunaweza kuligeuza kuwa umbo lolote tulitakalo, kwa nini hatutaki kujifunza kutokana na jinsi mama dunia anavyokuza viumbe vyake!,” anahoji mwanafalsafa huyo.
Jambo linguine, Froebel anafikiri kuwa ni muhimu kwa kila mlezi kuhakikisha kwamba mahitaji ya mtoto ya akili, vionjo na mwili yanatimilizwa katika kila kipindi cha kukua kwake.
Froebel pia alitilia mkazo vitendo kuliko nadharia, vitu vya kuchezea kuliko vitabu, stadi za mikono kuliko stadi za akili, mawazo yake yalifanana na yale ya ROSSEAU katika hili, lakini pia Froebel alitilia mkazo ujengaji wa uhusiano mwema kati ya watoto, jambo ambalo ROSSEAU hakutilia maanani.
Jambo jingine kubwa katika mawazo ya Froebel, linaoandamana na mawazo yake juu ya kukua kwa watoto ni kucheza. Anasema kuwa kucheza ni njia pekee inayokuza uwezo wa watoto kujifunza.
Anasema, “kucheza ndilo jambo bora kabisa katika maendeleo ya mtoto, kucheza ni kujieleza kwa mawazo na vionjo ambako hutokana na msukumo wa mtoto ulio ndani yake. Hii ndiyo maana ya neno kucheza.”
Anaendelea kusema kwamba katika kucheza, mtoto hukuza vipawa vitakavyojionyesha zaidi katika utu uzima, mtoto achezapo hujenga misingi ya tabia yake ya baadaye iwapo atakuwa mtu mpole au mkatili, mkarimu au mwenye choyo, mvivu au mwenye bidii, mpumbavu au mwerevu, mharibifu au mtunzaji vitu.
Pia, Froebel anazungumzia jambo alilotilia mkazo ROSSEAU yaani ubora wa kumshughulisha mtoto wakati anapojifunza (shughuli ya mtoto mwenyewe).
Alionyesha pia faida ya uongozi wa mwalimu na faida ya mtoto kujifunza pamoja katika vikundi vidogovidogo, au pengine kujifunza pamoja wakiwa darasa zima.
Alipendekeza pawe na uwiano wa kufaa kati ya kumwacha mtoto  kujishughulisha peke yake na kuongozwa na mwalimu, na pia kati ya kumwacha mtoto ajifunze peke yake au kumshirikisha na wenzake.
Kwa kweli madhumuni ya njia za kujifunzia alizopendekeza Froebel yalikuwa kuwapa watoto wapewe uzoefu wa kweli wa kisayansi, kwa kuanzia na upekuzi wa mambo yaliyowapendeza watoto wenyewe.
Mafunzo juu ya maumbile ya asili, kama vile sura ya nchi, mimea na wanyama yalipewa nafasi kubwa katika ratiba ya masomo na mara nyingi masomo yalifanywa nje ya darasa ili watoto waweze kuyaelewa mazingira yao.
Ijapokuwa Froebel alikazia jambo hilo la kujifunza kwa vitendo alionya pia kwamba katika kufanya vitendo vya aina mbalimbali watoto wasilazimishwe kushindana kwani si jambo zuri kumlinganisha mtoto mmoja na watoto wengine, badala yake kila mtoto ashindane na yeye mwenyewe yaani kila mara ajaribu kufanya vizuri kuliko alivyofanya mwanzo.

Imeandaliwa Na SIR ALMASI MICHAEL
                                         0758587116
                                         0656095123………………DAR ES SALAAM

Maoni 5 :

  1. Hongera mwl kwa kazi nzurii

    JibuFuta
  2. Nitumie azimio la elimu awali la mwaka huu kwenye WhatsApp 0766168794

    JibuFuta
  3. Tunaelimika sana kwaelim unayotupatia walimu tarajali tunaomba ututumie zaidi C/l,ICT na english activities

    JibuFuta
  4. Elimi ya awli inatakiwa pale tu mtoto anafikisha umri wa miaka 2 na nusu hadi sita, kwa umri wa 2 na nusu hadi 3 ajifunze kuimba na na kusoma kwa sauti mfano sauti T aseme T for Tree, ,tuwajali na serkali itandaze wingo moana wa elimu ya awli , by sir pascal

    JibuFuta

0656 095 123