Mwongozo wa mwalimu anayefundisha darasa la awali …ALMASI
MICHAEL
SIKU zote kunazungumzwa masuala ya
elimu ya awali na umuhimu wake, lakini kwa bahati mbaya elimu hii haitiliwi
maanani na ndiyo maana ukiwauliza watu 10 majina ya walimu wao wa awali ni
wawili tu watakaokumbuka.
Katika makala ya leo nitazungumzia
umuhimu wa elimu ya awali kwa kuangalia wanafalsafa makini walisema nini kuhusu
elimu hii, lakini kwanza tujikumbushe mwalimu wa elimu ya awali ni nani?
Mwalimu wa elimu ya awali anatakiwa
awe na msingi mzuri wa kitaaluma na kitaalamu ili aweze kutoa elimu iliyo
bora na kukidhi mahitaji ya watoto katika kujifunza.
Aidha, ufundishaji na kujifunza kwa
watoto hutokea katika njia mbalimbali— rasmi na zisizo rasmi— hivyo mwalimu wa
shule ya awali anahitaji maarifa na stadi za nyongeza ili kuwa mbunifu ili kila
mtoto apate msaada unaostahili.
Mtazamo wa elimu ya awali
Elimu ya awali ni elimu ambayo
inatolewa kwa ajili ya watoto wenye umri unaoanzia miaka 5-6. Lengo ni
kuwajengea watoto msingi mzuri wa kielimu ili kujiunga na elimu ya msingi.
Katika shule hizi watoto hujifunza
kwa kiasi kusoma, kuandika na kuhesabu. Wakiwa shuleni watoto hujifunza
ushirikiano na watu wengine, tabia njema, kazi za mikono na mambo mengine
yanayowasaidia katika makuzi.
Umuhimu wa elimu ya awali
Utafiti unaonyesha kuwa utoaji wa
elimu bora na stadi mbalimbali katika umri wa miaka 0-6 huchangia kwa kiasi
kikubwa maendeleo ya mtoto katika maisha yake yote.
Vilevile, elimu hii husaidia kubaini
matatizo mbalimbali ya watoto mapema ili wapatiwe msaada mapema kabla tatizo
halijawa kubwa. Pia taarifa hizi husaidia serikali kubuni mipango ya
kuwasaidia watoto hawa mapema.
Historia na maendeleo ya elimu ya awali Tanzania
Elimu ya awali nchini bado haijapiga
hatua kubwa, hata hivyo katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na kukua kwa
kasi kwa uanzishwaji wa shule za awali.
Elimu hii pia haijakua sana katika
sehemu za vijijini ambako ni sehemu chache mno zenye shule za awali kutokana na
upungufu wa walimu na mwamko duni wa wazazi.
Uamuzi wa hivi karibuni wa
serikali wa kuwa na shule ya awali katika kila shule ya msingi ya serikali
huenda ukachochea zaidi ukuaji wa elimu hii katika siku za hivi karibuni.
Elimu ya awali ilianza mwaka 1940
wakati wa kipindi cha ukoloni. Wakati huo elimu ya awali ilitolewa zaidi na
taasisi za kidini hasa zile za Kikristo na Serikali ya Kikoloni kwa watoto wa
tabaka maalumu.
Baada ya uhuru mwaka 1961, serikali
ilitoa nafasi kwa taasisi mbalimbali ili kuanzisha na kutoa elimu ya awali kwa
kufuata miongozo iliyowekwa.
Mwaka 1982 ripoti ya Tume ya
Rais Julius Nyerere, ilipendekeza kuwa elimu ya awali iingizwe katika mfumo
rasmi wa elimu, wizara ya elimu na utamaduni ilishauriwa iandae miongozo na
vifaa vya kufundishia na kujifunzia pamoja na kutoa mafunzo kwa walimu wa elimu
ya awali.
Miongozo ilitayarishwa mwaka 1991 na
wizara ya elimu lakini kwa kuwa hakukuwa na chombo cha kufuatilia utekelezaji
wake, shule nyingi zilitoa elimu ya awali bila kuzingatia viwango
vinavyostahili.
Mwaka 1995, Sera ya Elimu na Mafunzo
ilitolewa na kuelekeza kuwa elimu hii itatolewa kwa watoto wa miaka 5-6 na
itasimamiwa na wizara.
Nadharia mbalimbali kutoka kwa wanafalsafa kuhusu elimu ya
awali
MARIA MONTESSORI (1870- 1952)
Alizaliwa Italia; alikuwa mwanamke
wa kwanza nchini humo kuwa daktari wa magonjwa ya watoto na magonjwa ya akili.
Katika ugunduzi wake, alingundua
kuwa watoto waliovia akili wanaweza kufunzwa kwa kutumia vifaa vya kuchezea
wanavyovipenda. Aliamini kuwa tatizo la kuvia akili ni la kielimu na sio la
tiba.
Montessori, aliamini kuwa elimu ya
mtoto ni lazima ianze mapema sana kwa sababu umri wa mtoto kati ya
kuzaliwa hadi miaka sita ni muhimu sana kwa ujenzi wa haiba yake.
Alipendekeza mwalimu atumie vifaa
vingi katika ufundishaji, vifaa hivyo viwe ni vile vinavyokuza tabia ya udadisi
na ugunduzi, vinavyompa nafasi ya utendaji na vinavyomwezesha mtoto kufanya
majaribio, kutatua vikwazo, ujasiri, kuuliza na kujibu maswali, kupenda
kufaulu, kujiendeleza na kumpa msukumo wa kujitegemea katika utendaji.
Mwanafalsafa huyo hakuishia hapo, bali
alibuni michezo ya kujifunzia, alitumia vifaa vya kuchunguza ambavyo humpatia
mtoto maarifa na hapo hapo kukuza stadi wakati anapovichezea.
Kuhusu vyumba vya madarasa ya awali,
alipendekeza vigawanywe katika vyumba vingi na kila chumba kiwe kwa ajili ya
kufanyia shughuli maalumu tofauti, watoto wawe huru kutembea na kuingia kila
chumba wakitakacho bila kizuizi.
Wanafunzi wajifunze kwa kushirikiana
na hali inayotakiwa mle vyumbani iwe ya kuheshimu haki na kazi za kila
mtu.Watoto wadogo wajifunze kutoka kwa wenzao walio wakubwa, vifaa vilivyomo
katika nyumba kwa mfano viti vya kukalia viwe vidogo kama walivyo watoto
wenyewe.
MONTESSORI, anajulikana sana
kwa kuwa mtu aliyeanzisha njia ya kuwafundisha watoto wadogo.Njia yake ya
kufundishia watoto wadogo aliigawa katika sehemu kuu zifuatazo:
- Elimu inayohusu ukuzaji wa stadi mbalimbali za misuli ya watoto. Elimu hii ni nzuri kwa kumsaidia mtoto aweze kukuza stadi zake na kufikia upeo wa juu katika kutumia viungo vya mwili. Ili kufikia hali hii, wanafunzi wafanye mazoezi mbalimbali ya kutembea na kupumua.
Pia,
alitumia elimu ya mazoezi yanayohusiana na maisha ya kila siku ya mtoto kwa
mfano usafi wa mwili, usafi wa mazingira ya ndani na nje.
- Elimu inayohusu ukuzaji wa milango ya fahamu, mazoezi aliyoyapendekeza kwa watoto ni yale ya kuwasaidia watoto kuweza kutofautisha kati ya uwingi na ubora wa kitu, mazoezi yanayotumiwa katika elimu hii ni yale ya kuona na kusikia.
- Elimu inayohusu weledi, mazoezi ya kuwapa wanafunzi ni yale ya kumtayarisha mtoto kusoma kuandika na kuhesabu, kwa mfano mtoto huanza kugusa, kuangalia, kuandika na hatimaye kusoma.
Vifaa ni
vya lazima sana kwa kukuza elimu ya aina hii, vifaa hivyo ni kama vile shanga
za rangi mbalimbali, vizibo vya chupa, vipande vya miti vilivyoandikwa namba, alfabeti
zinazoweza kusogezwa au mbegu za mimea.
JEAN JACQUES ROSSEAU (1712-1778)
Alizaliwa mwaka 1712 katika mji wa
Geneva huko Uswisi ambako alipata mafunzo yake ya awali kutoka kwa baba yake na
baadaye kutoka kwa mkufunzi aliyeajiriwa kumfundisha.
ROSSEAU alikuwa na mwelekeo wa
kuamini kuwa kwa asili watoto huzaliwa na tabia nzuri na kwamba ni mazingira
ndiyo yanayowafanya kuwa na tabia mbaya.
Alisisitiza njia bora ya
kuwaelimisha watoto ni kuwaweka katika hali ya asili ambayo itamwezesha
kukuza tabia, silika zao za uwezo bila kuathiriwa na mazingira.
Aligawanya maisha ya mtoto katika
hatua nne;
- Hatua ya kwanza ni ya mtoto mchanga. Huu ni wakati mtoto anapojenga mazoea na tabia njema, ni wakati unaofaa kumwongoza mtoto kutawala maono yake.
- Hatua ya pili ni wakati wa kujifunza namna ya kutumia milango yake ya fahamu au maarifa.
- Hatua ya tatu ni mwanzo wa uvulana au usichana, hiki ni kipindi cha akili mtoto anapotumia akili yake juu ya vitendo anavyofanya.
- Kipindi cha nne ni uvulana au usichana mpevu (baada ya miaka 15), hiki ni kipindi cha fikra za kiroho, hapo mtoto anatambua hasa mema na mabaya.
ROSSEAU alieleza umuhimu wa mtoto
kuwa kitovu cha elimu ili kumpa hali nzuri ya maisha. Alisisitiza kuwa elimu
lazima imsaidie mtoto kuwa huru na mwenye furaha, elimu imsaidie mtoto kukuza
haiba nzuri, na ili elimu ifikie malengo haya lazima itolewe kufuatana na hali
na hatua za kukua kwa mtoto.
Mtoto afundishwe namna ya kujifunza
na kutatua matatizo katika mazingira malimbali, alisisitiza kuwa elimu ni haki
ya watoto wote ni chombo kinachoweza kuyatawala mazingira ya mtoto.
Alishauri kuwa ufundishaji
uende sambamba na hatua za ukuaji wa mtoto, uzingatie upevu na utayari wa mtoto
katika kujifunza.
Njia bora za kufundishia ni zile
zinazomsaidia mtoto kutumia milango mingi ya fahamu inavyowezekana. Ili
kufanikiwa katika jambo hili mwalimu atumie zana za kufundishia hasa kwa
kutumia vitu halisi.
Kwa mujibu wa mwanafalsafa huyu,
elimu lazima izingatie mahitaji ya maadili, katika falsafa ya elimu ya
kujitegemea ufundishaji wa maadili umezingatiwa kwa kuwafundisha wanafunzi
masomo ya siasa na dini.
JOHN DEWEY
Huyu alizaliwa mwaka 1859 huko
Vermont, Marekani na alifariki mwaka 1952 akiwa na umri wa miaka 93.
Mwanafalsafa Dewey, aliandika mengi na kufanya mengi yaliyomtambulisha kidunia
kuwa ni mtaalamu wa falsafa na mwalimu hodari hasa katika nadharia inayohusu
malezi ya watoto.
Kutokana na kazi ya Dewey
zilianzishwa shule zilizojulikana kama shule za maendeleo, na malezi
yaliyotolewa yakaitwa malezi ya
maendeleo.
Akiwa jimbo la Michigan, Dewey
alianzisha kituo cha watoto wadogo alichokiita shule ya maabara mwaka
1896, alikusudia shule hiyo itoe nafasi ya kufanya utafiti na majaribio juu ya
namna ya kujifunza.
Dewey alisisitiza kuwa elimu haiwezi
kutengwa na jamii, kwa hali hiyo basi, elimu ni njia ambayo jamii huitumia
katika kulinda, kuendeleza na kuhifadhi utamaduni wake.
Madhumuni ya elimu basi ni
kutayarisha na kutoa raia walio bora na wanaoweza kuitumikia jamii yao
kikamilifu.
Dewey aliamini kuwa katika kutenda
au kufanya shughuli fulani, wanafunzi wanaweza kuelewa mambo vizuri zaidi.
Alisisitiza kuwa maarifa hupatikana kutokana na shughuli wazifanyazo watoto.
Kuhusu suala la kujifunza, Dewey
alitaja mambo ambayo ni muhimu kuzingatia wakati wa kumfundisha mtoto. Mambo
hayo ni haya yafuatayo;
- Mwanafunzi lazima awe katika mazingira halisi ya aina ya uzoefu anaotakiwa kupata.
- Lazima kuweko na tatizo la kweli linaloamsha na kuchochea mawazo na ari ya mwanafunzi ya kutatua matatizo.
- Mwanafunzi lazima afanye uchunguzi na atafute au akusanye data za kumsaidia katika kulitatua tatizo lake.
- Ni lazima ajaribu kutafuta ufumbuzi mbalimbali wa tatizo hilo.
- Ni lazima apate muda wa kufanya majaribio kuona kama mawazo au dhanio alizozipata ni kweli zinaweza kuwa na uthibitisho wowote.
Dewey alilisisitiza kuwa shule iwe
kaya njema ambamo mtoto atafundishwa maadili yote ya jumuiya yake, na kumjenga
kimwili na kiroho.
FRIEDRICH FROEBEL
Froebel anashika nafasi ya pekee
kati ya wataalamu wa mambo ya malezi, ijapokuwa mawazo yake makuu yalifanana na
yale ambayo ROSSEAU alikuwa amekwisha kuyaandika.
Alizaliwa Ujerumani mwaka 1782
katika kijiji kilichokuwa katika msitu wa Turingia. Akiwa kijana bado alifanya
kazi chini ya uangalizi wa Bwana Misitu na kwa nafasi hiyo alijipatia moyo wa
kupenda uoto wa asili juu ya sura ya nchi, na pia kupenda maumbile ya asili ya
nchi.
Sifa kuu ya Froebel imo hasa katika
kuzua wazo la kuwa na shule za Chekechea (Kindergarten). Jina hili la
Kindergarten ambalo lina maana ya “bustani ya watoto” ndilo hasa lililoeleza
imani na msimamo wa Froebel juu ya malezi.
Yeye alimlinganisha mtoto na mmea
mchanga, na kazi ya mwalimu akailinganisha na kazi ya mkulima bustani ambaye
wajibu wake ni kutengeneza mazingira yanayofaa ili mmea ukue wenyewe hata
kufikia kikomo chake.
Mawazo yake kuhusiana na elimu na
jinsi ya kumuandaa mtoto kielimu ni haya yafuatayo:
Froebel alipendekeza pawe na umoja
katika mambo yanayofundishwa na kutaka tuepuke hatari ya kuyagawa masomo katika
sehemu ndogondogo zisizohusiana, kwa mfano yeye alihimiza kuwa mitaala ya
masomo ionyeshe umoja.
Aliwalaumu pia walimu wa vyuo vikuu
ambao walikuwa wameligawa somo la malezi katika sehemu nyingi ili waandike
vitabu.
Alisema pia katika shughuli ya
malezi, uhuru wa mtoto ni muhimu uzingatiwe, “Sisi binadamu tunapotunza mimea
na wanyama tunawaachia nafasi ya kujimudu na pia muda wa kukua.
“Lakini mtoto wa binadamu tunamfanya
kama kipande cha nta au donge la udongo, ambalo tunaweza kuligeuza kuwa umbo
lolote tulitakalo, kwa nini hatutaki kujifunza kutokana na jinsi mama dunia
anavyokuza viumbe vyake!,” anahoji mwanafalsafa huyo.
Jambo linguine, Froebel anafikiri
kuwa ni muhimu kwa kila mlezi kuhakikisha kwamba mahitaji ya mtoto ya akili,
vionjo na mwili yanatimilizwa katika kila kipindi cha kukua kwake.
Froebel pia alitilia mkazo vitendo
kuliko nadharia, vitu vya kuchezea kuliko vitabu, stadi za mikono kuliko stadi
za akili, mawazo yake yalifanana na yale ya ROSSEAU katika hili, lakini pia
Froebel alitilia mkazo ujengaji wa uhusiano mwema kati ya watoto, jambo ambalo
ROSSEAU hakutilia maanani.
Jambo jingine kubwa katika mawazo ya
Froebel, linaoandamana na mawazo yake juu ya kukua kwa watoto ni kucheza.
Anasema kuwa kucheza ni njia pekee inayokuza uwezo wa watoto kujifunza.
Anasema, “kucheza ndilo jambo bora
kabisa katika maendeleo ya mtoto, kucheza ni kujieleza kwa mawazo na vionjo
ambako hutokana na msukumo wa mtoto ulio ndani yake. Hii ndiyo maana ya neno
kucheza.”
Anaendelea kusema kwamba katika
kucheza, mtoto hukuza vipawa vitakavyojionyesha zaidi katika utu uzima, mtoto
achezapo hujenga misingi ya tabia yake ya baadaye iwapo atakuwa mtu mpole au
mkatili, mkarimu au mwenye choyo, mvivu au mwenye bidii, mpumbavu au mwerevu,
mharibifu au mtunzaji vitu.
Pia, Froebel anazungumzia jambo
alilotilia mkazo ROSSEAU yaani ubora wa kumshughulisha mtoto wakati
anapojifunza (shughuli ya mtoto mwenyewe).
Alionyesha pia faida ya uongozi wa
mwalimu na faida ya mtoto kujifunza pamoja katika vikundi vidogovidogo, au
pengine kujifunza pamoja wakiwa darasa zima.
Alipendekeza pawe na uwiano wa kufaa
kati ya kumwacha mtoto kujishughulisha peke yake na kuongozwa na mwalimu,
na pia kati ya kumwacha mtoto ajifunze peke yake au kumshirikisha na wenzake.
Kwa kweli madhumuni ya njia za
kujifunzia alizopendekeza Froebel yalikuwa kuwapa watoto wapewe uzoefu wa kweli
wa kisayansi, kwa kuanzia na upekuzi wa mambo yaliyowapendeza watoto wenyewe.
Mafunzo juu ya maumbile ya asili,
kama vile sura ya nchi, mimea na wanyama yalipewa nafasi kubwa katika ratiba ya
masomo na mara nyingi masomo yalifanywa nje ya darasa ili watoto waweze
kuyaelewa mazingira yao.
Ijapokuwa Froebel alikazia jambo
hilo la kujifunza kwa vitendo alionya pia kwamba katika kufanya vitendo vya
aina mbalimbali watoto wasilazimishwe kushindana kwani si jambo zuri
kumlinganisha mtoto mmoja na watoto wengine, badala yake kila mtoto ashindane
na yeye mwenyewe yaani kila mara ajaribu kufanya vizuri kuliko alivyofanya
mwanzo.
Imeandaliwa Na SIR ALMASI MICHAEL
0758587116
0656095123………………DAR ES SALAAM