Ijumaa, 8 Machi 2019

Haya Ndio Maendeleo Anayofanya Mchezaji Samatta Huku Tanzania na Mamilioni Anayopata Huko Ulaya

Samatta amejenga msikiti mkubwa katika Wilaya ya Mkuranga, Tarafa ya Vikindu, Kata ya Kidubwa Mkoa wa Pwani, wenye uwezo wa kuingiza jumla ya waumini 5,000 upande wa wanaume ni 3,000 na wanawake 2,000.

HUYU Mbwana Samatta msimchukulie poa mjue! Wengi tunamjua kutokana na umaarufu wake wa kusakata soka katika Klabu ya KRC Genk ya Ubeligiji.

Lakini kwenye mambo ya kijamii ndio usipime unaambiwa anafanya mambo makubwa yasiofahamika na wadau wa soka ndani na nje ya nchi.

Kitu kinachomfanya Samatta atikise kwenye soka ni namna anavyojua kucheka na nyavu, hadi sasa amefikisha mabao 20 kwenye Ligi Kuu ya Ubeligiji ‘Jupiter Pro’ na mabao tisa kwenye Europa League.

Mambo yake mengi hayafahamiki kwasababu jamaa si si mtu kujionyesha. Samatta ni msiri mno.

Mwanaspoti limeona likufahamishe usiyoyajua kuhusu supastaa huyo anayoyafanya nje ya uwanja, kubwa zaidi ameajiri vijana wengi kupitia miradi yake mbalimbali.

Samatta amefungua kampuni ya utalii inayojulikana kwa jina la Mbwana Samatta Touries and safaris. Tayari imepata vibali vyote vya serikali kinachosubiriwa ni vitendea kazi.

Baba mzazi wa staa huyo, Ally Samatta Pazi anafunguka mikakati inayoendelea kuhusiana na kampuni hiyo inayotarajiwa kufanya kazi wakati wowote kuanzia sasa.

Mzee Pazi anasema tayari gari moja limeishanunuliwa ni aina ya Alphard ambalo linaenda kubadilishwa namba kutoka kwenye usafiri wa kutembelea na kuwa la biashara.

“Hapa magari yanayosubiriwa ni matatu ambayo ni ya kitalii na yapo njiani tunasubiri muda wa kufika Tanzania. Samatta ameishamwajili mkurugenzi mkuu anayeitwa Khamis Waziri ambaye ana uzoefu na kazi hiyo kwa muda wa miaka tisa, msaidizi wake Hazibun Habibu.

“Vituo vitakuwa viwili Arusha ambako ndiko atasimamia mkurugenzi mkuu Waziri na Dar es Salaam atasimamia msaidizi wake Habib,”anasema.

Mzee Pazi anaendelea kulimwagia siri Mwanaspoti kwamba ajira zitakuwa nyingi kwenye kampuni hiyo kama kuajiri wapishi, wafanya usafi, walinzi, madereva, wapokea wageni ‘receptionist’ na katibu.

“Itaajiri watu wenye umri tofauti, hiyo ni ajira tosha kwa Watanzania wenzake pia yatakapofika hayo magari tutafanya ufunguzi kwa kualika watu mbalimbali wakiwemo kutoka serikalini ili kutia mkono wa baraka.

“Pia, katika uzinduzi huo ameniambia atakuja na wachezaji wenye majina makubwa duniani, lakini wa timu ambayo atakuwepo kwa wakati huo, hivyo hakutaka kufunguka majina yao,”anasema.

Mzee huyu anaongeza ofisi ya Samatta itakuwa kwenye nyumba yake iliopo Kibada ambapo atakuwa anasikiliza mambo ya utalii pamoja na masuala ya mikataba ya wachezaji kwa hiyo kuna vitu vingi vikubwa anavyotaka kuvifanya,”anasema.

Samatta amejenga msikiti mkubwa katika Wilaya ya Mkuranga, Tarafa ya Vikindu, Kata ya Kidubwa Mkoa wa Pwani, wenye uwezo wa kuingiza jumla ya waumini 5,000 upande wa wanaume ni 3,000 na wanawake 2,000.

Msikiti huo una mabafu sita na vyoo sita kwa wanaume na kwa wanawake vivyo hivyo, kuna sehemu ya kuchukulia udhu( kutawaza) kwa wanawake na wanaume, ofisi ya imamu na chumba cha kuoshea maiti.

“Msikiti ulipofikia watu wanaweza wakaswali kwa sababu una kila kitu kinachostahiki kwa maana ya maji ya kutosha na vyumba, mabafu na vyoo vipo kamili ingawa unaendelea kuutengeneza ili uwe wa kisasa zaidi.

“Yupo kwenye mchakato wa kununua spika za ndani na za juu kubwa kwani kilichobaki ni kumalizia sakafu za chini, plasta, madirisha na milango,”anasema.

Alipoulizwa nani wamemteua kuwa imamu wa msikiti, Mzee Samatta anajibu: “Kuhusu nani atakuwa imamu mkuu wa msikiti sijajua bado naelewa kuhusu ujenzi tu na vyumba vyake hilo litajulikana badaye,”anasema.

Anaelezea msikiti huo umejengwa kwa gharama si chini ya 5000 milioni na kudai zinaweza zikaongezeka baada ya kukamilisha kila kitu kilichobakia.

“Pesa zimetumika nyingi kikubwa nashukuru ni kwa sababu ya Mungu ambaye anampa nguvu za kufanya kazi ya soka kuwa Samatta ambaye mnamjua kwa sasa,”anasema.

ULINZI SAsa KWENYE MJENGO WAKE

Samatta ametoa ajira nyingine kwa vijana wenzake, ameajiri kampuni ya ulinzi inayojulikana kwa jina Nanga, hivyo ukifika kwenye mjengo huo bila kibali maalumu cha baba yake mzazi ujue umeumia.

Kampuni hiyo ipo makini kufanya kazi ya kuhakikisha nyumba za staa huyo zinakuwa salama na vitu vilivyo ndani yake. Hivi karibuni walimkamata kijana mmoja waliyemtaja kwa jina la Mwinjuma ambaye alikuwa ameruka ukuta kwenda kuiba taa.

Kijana huyo unaambiwa alishushiwa kichapo cha maana kisha akampelekwa polisi.

Kijana ambaye ni mtunza stoo wa Samatta, aliyejitambulisha kwa jina la Clement Lucas amesimulia tukio zima lilivyokuwa “Tofauti na zamani hii kampuni ya ulinzi Nonga iko makini, huyo kijana alidhibitiwa cha ajabu na sasa amefungwa miezi sita.

“Kuna kijana mmoja alikuwa akilinda kabla ya Kampuni ya Nonga kuajiriwa, kulipobainika kuwepo kwa upotevu wa vitu akafukuzwa kazi, kwa sasa bila kibali cha familia ya Samatta hapa huruhusiwi kukanyaga,” anasema.

Mtunza stoo huyo wa Samatta amefunguka jinsi staa huyo alivyobadilisha maisha yake.

“Tangu nimeajiriwa na yeye nimenunua uwanja jijini Arusha ingawa kuna pesa ambayo bado nadaiwa ameniambia atamalizia, mbali na hilo kila akija Tanzania, basi wafanyakazi wake tunaogelea neema ni kijana ambaye ana huruma na kusikiliza shida zetu kwa utulivu,”anasema.

MABADILIKO YA NYUMBA YAKE

Tayari ameishaweka vioo, huku baadhi ya vyumba kuendelea na ukarabati kama jikoni kuweka makabati, malumalu, kufunga taa na umeme upo tayari ndani ya nyumba hiyo.

Mzee Samatta anasimulia na huku Mwanaspoti linashuhudia anachokieleza kwa kuonyesha “Hii ni ofisi yake ipo juu ambako ni sehemu yake kwa maana ya masta, ofisi hii itakuwa inajihusisha na vitu vingi.

“Kuna watu ambao ameishawatafutia kazi ndani na nje ya nchi siwezi kuwaweka wazi labda aje ataje mwenyewe, ndio maana amefungua ofisi ambayo atakuwa akipatikana kwa ajili ya kuhudumia jamii.

“Pia, amenigusia kwamba atakuwa anashugulika na masuala ya mikataba ya wachezaji nadhani ana vitu vingi vikubwa. Hii nyumba juu ina vyumba vitatu nje ya masta yake na chini viwili, msikiti, jiko, sebule, stoo na vitu vingine.

“Lakini pia ina jumla ya vyoo vitano, achilia mbali vile vya nje kabisa ambavyo ni viwili na mabafu mawili pamoja na sehemu ya kuhifadhia matenki ya maji,”anasema.

Samatta si mwenzio thamani zake za ndani zote ameziagiza kutoka China, tayari kuna vitanda, magodoro, friji, masofa na makabati ya jikoni.

“Yaani hapa kila kitu kipo tayari kwa maana ya vifaa vya ujenzi na thamani za ndani, ukarabati ukimalizika zitaanza kuwekwa thamani za ndani ambazo wataajiriwa watalamu wa kupangilia,”anasema Mzee Samatta.

GHARAMA ZA UJENZI USIPIME

Awali Mwanaspoti lilitembelea nyumba hiyo na kukuta baadhi ya vyumba havijawekwa malumalu, thamani za ndani zilikuwa bado, lakini baba yake alilieleza kilitumika kiasi cha 1.5 bilioni kufanya kazi hiyo.

Ilipofikia nyumba hiyo kwa sasa Mzee Samatta anafunguka pesa zilizotumika sio chini ya 300 milioni.

“Anapambana ingawa sipendi kuzungumzia mambo ya gharama na yeye hataki kabisa,”anasema.

Mzee Samatta anasema mwanaye huyo amenunua madaladala mawili ambayo yapo chini yake.

“Unajua hakuniambia moja kwa moja baada ya kununua badaye akaja kusema baba utakuwa unapata vihela vya mbogamboga.

“Lakini pia kwenye daladala hizo kumeajiriwa watu ambao wanapata kipato cha kujikimu na maisha yao, naona bado anaendelea kujihusisha na jamii ingawa sio msemaji sana wa mambo hayo,”anasema.

Anasema alikuwa na Bajaj tano, nne kawapa kaka zake na moja mtarajiwa wake ambaye amezaa naye watoto wawili Karimu (4) na wa kike Isimini (2).

“Kuna vitu ambavyo ameamua kupunguza majukumu ndio maana amegawa hizo Bajaj kwa lengo la ndugu zake wajitegemee, wanazifanyia biashara hivyo yeye anahusika na vitu vikubwa vikubwa,”anasema.

Pamoja na kuwa na nyumba nyingi ambazo anafanya biashara ya kuzipangisha na mjengo wa maana aliyojenga, Samatta amepanga nyumba ya Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete iliopo Kijichi, anafichua mzee wake.

“Baada ya kukamilisha kila kitu huku ndani ndipo atakapohamisha familia yake, ndio maana ameweka ulinzi wa kutosha na bila kibali ukifika hapa unaweza ukapata matatizo,”anasema.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

0656 095 123