Vifahamu Vitu Vidogo Vidogo Ambavyo Huzidisha Utamu wa Mahusiano Katika Mapenzi
MAPENZI ni matamu, mapenzi yana raha yake haswa ukimpata mtu anayekupenda kama ambavyo wewe unampenda. Kinyume chake, mapenzi hugeuka kuwa shubiri. Yanaumiza lakini suala la msingi, hupaswi kukata tamaa pindi unapokutana na penzi kuwa chungu. Chukulia ni changamoto, usikubali kuishi kwenye majonzi kwa muda mrefu. Amini akili yako ina majibu juu ya changamoto inayokukumba na pia unaweza kuiepuka.
Unapoamini kwamba changamoto inaweza kupita, utaifanya akili yako iwaze kupata majibu ya haraka iwe ni kusaka suluhuhisho kwa kuzungumza na mwenzi wako na unapoona maji yamezidi unga basi ni bora ukajiweka pembeni hususani mnapokuwa katika hatua za awali.
Nimeanza kuyasema hayo maana katika uhusiano wowote, kikubwa kinachotafutwa na wapendanao huwa ni furaha ya moyo. Wapendanao wanapaswa kuishi kwa furaha, amani na upendo. Uhusiano wao uwe sehemu ya kudumisha urafiki, udugu na kwa pamoja muweze kuishi vizuri.
Wapendanao wanatengeneza umoja wao ambao ni wa kutiana moyo pale mambo yanapokuwa si mazuri. Wakati wa matatizo na wakati wa furaha wanakuwa pamoja, wanategemeana katika kuifanya safari yao ya hapa duniani iweze kutimia sawasawa na mpango wa Mungu.
Kwa kuzingatia hilo, kila mmoja anapaswa kuwa furaha ya mwenzake. Anapaswa kumtendea mambo mazuri ili aweze kuwa na furaha na amani muda wote. Mwanaume anapaswa kushughulikia amani na furaha ya mwanamke wake, vivyo hivyo mwanamke ashughulikie furaha na amani ya mwanaume wake. Kuna vitu ambavyo mara nyingi huwa tunaviona ni vidogo lakini kimsingi huwa vina maana kubwa sana katika suala zima la uhusiano wa kimapenzi kwa mchumba au hata hatua ya ndoa.
MITOKO
Mara nyingi wapendanao huwa wanajisahau sana katika suala zima la mitoko ya hapa na pale. Mara nyingi kila mtu anajua kutoka kivyake na marafiki zake.
Mwanaume anatoka kwenda hoteli au sehemu mbalimbali za burudani na rafiki zake na mwanamke naye anatoka na mashoga zake. Ndugu zangu, hata kama kweli kila mtu ana mitoko yake lakini ni vyema kujiwekea utaratibu siku moja moja wapendanao mkatoka pamoja, ina maana kubwa sana.
ZAWADI
Lingine ni la vizawadi. Hata kama unajua kwamba mwenzako ana uwezo wa kununua kile ambacho wewe utamnunulia lakini fanya hivyo kama ishara ya upendo, inaleta maana kubwa sana katika uhusiano.
MPE KIPAUMBELE
Unapokuwa unawaza juu ya jambo fulani, mpe kipaumbele mwenzi wako kwa kuomba hata ushauri badala ya kuomba ushauri kwa marafiki zako, wafanyabiashara au wafanyakazi wenzako. Mwenzi wako anapoona humpi kipaumbele hususani katika masuala ya msingi, anaweza kuona ni kama unamdharau na hivyo kupunguza hamu ya kuwa na wewe.
MSAIDIE
Kuna wakati mwenzi wako anaweza kuwa anaweza kufanya jambo fulani lakini anapokuwa na wewe, anatamani wewe umsaidie, hilo nalo lina maana kubwa lifanye kadiri uwezavyo.
MJALI
Hili ni la muhimu sana, unaweza kuona kama halina maana sana lakini unapokuwa unamkumbusha mwenzi wako kuhusu suala la kula au kumuamsha asubuhi awahi kazini na mambo mengine kama hayo, yanaleta chachu na hamasa kubwa katika uhusiano.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
0656 095 123